Friday, September 9, 2011

Simba Sc 1-0 Villa Squad Fc

Issa Mnally na Khatimu Naheka
BAO lililofungwa na mshambuliaji wa Simba, Gervais Kago, lilisababisha kuibuka kwa vurumai kubwa ndani ya Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga juzi Jumatano.

Vurumai hizo ziliibuka katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Villa Squad. Mashabiki wa Simba walianza kushangilia bao hilo lakini walikutana na upinzani mkali kutoka kwa wale waliokuwa wakiiunga mkono Villa.

Ghafla kulitokea mvutano na kukunjana mashati baina ya mashabiki wa Simba na wale wanaosemekana kuwa ni wa Yanga ambao hiyo juzi walikuwa wakiiunga mkono Villa.

Tafrani hizo ziliendelea kwa takribani dakika tano kabla ya mashabiki waungwana kujitokeza na kuwatuliza wenzao ambao hata baada ya kukubali waliendelea kutoleana lugha chafu, huku kila upande ukijigamba wao ni bora zaidi.

Katika mechi hiyo, Simba ilishinda kwa bao hilo moja lililofungwa katika dakika ya saba na raia huyo wa Afrika ya Kati.

Wakati huo huo, juzi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, mashabiki waliodaiwa kuwa ni wa Yanga waliugeuza uwanja huo kuwa sehemu ya mapambano baada ya kuwarushia mawe wenzao wa Simba waliokuwa wakiishangilia Mtibwa Sugar mara baada ya mechi hiyo.

Tukio hilo lilitokea baada ya mashabiki wa Yanga kuchukizwa na kutendo cha timu yao kutoka suluhu dhidi ya Mtibwa katika mechi hiyo ya ligi kuu.
Mashabiki hao walirusha mawe hayo wakati walipokuwa wakitoka uwanjani na kusababisha amani kupotea kwa dakika kadhaa.

Kutokana na tukio hilo, wachezaji na Kocha wa Mtibwa, Tom Olaba, waliokuwa wakijikusanya kabla ya kuondoka uwanjani hapo, walitawanyika na kuanza kukimbilia kwenye magari ili kujinusuru na mawe hayo.

Hata hivyo, hali hiyo ilitulia baada ya askari kuwatawanya mashabiki waliokuwa wakirusha mawe. Mpaka Championi Ijumaa linaondoka uwanjani hapo, hakukuwa na yeyote aliyejeruhiwa.

....kwa msaada wa mtandao wa globalpublishers.

0 comments:

Post a Comment